Monday 5 September 2016

MSIMU WA PILI WA RIWAYA YA MWANAFUNZI MCHAWI SEHEMU YA 1


Riwaya: MWANAFUNZI MCHAWI
(MSIMU WA 2)
MTUNZI:ENEA FAIDY

SEHEMU YA KWANZA.

Watu wengi nchini Tanzania walikuwa wametulia tuli kutazama runinga zao majira ya Saa moja kamili jioni. Kwani kipindi kizuri chenye simulizi ya kweli na ya kusisimua kutoka

. kwa Doreen Mbwana kilikuwa kikiendelea katika kituo kimoja cha televisheni maarufu sana nchini kilikuwa kinarusha matangazo yake mubashara kutoka hospitali aliyokuwa amelazwa Doreen.
Wanafunzi wa shule ya Mabango ambao walikuwa wamefunga shule siku ile ya Ijumaa walikuwa bwaloni wakitazama televisheni kwani hawakuruhusiwa kuondoka kwa siku ile na utaratibu wao ilibidi waondoke Siku ya kesho yake . kwa hivyo walokuwa na Uhuru wa kutazama televisheni kadri wawezavyo.
Maandishi makubwa yaliyokolezwa kwa wino wa bluu yalipita chini ya kioo cha televisheni na yakazidi kuwatia hamasa wanafunzi wale ili waweze kutazama kwa umakini kipindi kile."KAA TAYARI KWA KIPINDI MAALUMU KUTOKA KWA DOREEN MBWANA AKIELEZEA CHANZO CHA YEYE KUWA MCHAWI" 
Tangazo hilo lilikuwa na nguvu ya kuwavuta watazamaji wengi na kutulia kama maji ya mtungini ili waweze kusikia vizuri na kwa umakini mkubwa.

Umakini huo haukuwa kwa wanafunzi na walimu wa Mabango pekee bali ni nchi nzima. Familia ya akina Pamela ilikuwa imetulia tuli na  kwa mshangao wa hali ya juu wakisubiri kusikia kitu kutoka kwa Doreen.
Pia Mwalimu John na familia yake hawakuacha kukodoa macho yao kwa umakini sana ili wasipitwe na neno lolote kutoka kwa Doreen Mbwana. 

Haukupita muda mrefu sana picha ya Doreen ilitanda kioo kizima cha televisheni na alikuwa tayari kuanza kipindi huku machozi yakimbubujika kwa kasi mashavuni mwake lakini akaamua kujikaza kisabuni kwa kujifuta machozi Ili aweze kuzungumza vizuri na kusikika kwa watazamaji wake.
Kamera ilienda moja kwa moja kwenye majeraha makubwa ya Doreen yaliyositiriwa kwa bandeji kisha ikauweka sawa USO mzuri wa Doreen ambao ulichakazwa kwa kilio cha muda mrefu pamoja na vipigo. Muda wa Doreen kujieleza yw moyoni ukawadia akakohoa kidogo kisha akaanza kuuambia umma kile alichokusudia kukisema.

"Ni aibu kubwa sana kwa binti mdogo kama Mimi Doreen, kupata tuhuma za uchawi tena si kidogo Bali kwa kuangamiza watu wengi sana wasiokuwa na hatia na kuwaharibu binadamu ambao hawakunikosea kitu. Nakiri kuwa na makosa makubwa sana tena nakiri kuwa Mimi ni zaidi ya mnyama wala sistahili adhabu yoyote zaidi ya kifo... Roho yangu inanisuta sana ndio maana nimeamua kutangaza hili ili walau nijipunguzie mzigo mzito nilioubeba.. Najuta sana! Naomba radhi kwa Mola wangu pia kwa wote niliowakosea" alisikika Doreen kwa sauti iliyojaa uchungu na simanzi akijutia kile alichokifanya kwa muda mrefu.
"Nitasimulia maisha yangu kwa ujumla... Nanyi mtakuwa hakimu na kunihukumu kadri ya vile ninavyostahili... Mengi sikuyajua ila nilisimuliwa na mama yangu Bi Hamisa Hamis... Kwa namna moja au nyingine naweza sema namchukia sana mama! Najuta ni kwanini alinizaa!" Alisema Doreen kauli hiyo tata iliyowaacha watu wengi midomo wazi na kumwona Doreen kama binti asiye na adabu hata kidogo! Kwanini atamke wazi kuwa hampendi mama yake wakati alimbeba tumboni kwa takribani miezi Tisa? Tena akamlea kwa mapenzi mazito hatimaye akawa binti mkubwa tena mzuri kupita kiasi?
Doreen alishusha chozi lake kisha akaanza simulizi yake ya kusisimua sana.

******
Kumbukumbu zikarudi nyuma sana mpaka miaka 20 iliyopita kama ambavyo Doreen alisimuliwa na mama yake.

Katika wilaya ya Pangani mkoani Tanga ndiko alikokuwa akiishi Bi Hamisa Hamisi ambapo alitokea katika familia duni sana ya Bwana Hamisi Mandevu. Binti Huyo aliyekuwa na uzuri wa aina yake alipata bahati ya kuolewa na mfanyabuashara maarufu sana mkoani humo aliyefahamika kwa jina la  Adrian Mbwana. Kiukweli ilikuwa bahati kubwa sana kwa Hamisa kwani mumewe angekuwa chanzo cha kuiinua familia yake kiuchumi. 

Licha ya kwamba Bwana Adrian Mbwana alikuwa na dini tofauti na Hamisa Hilo halikuwa tatizo kabisa kwani mapenzi mazito yaliyochipua haina yao yalikuwa na nguvu tosha ya kuzivunja tofauti zao za kidini.
Licha ya kwamba Bwana Hamis Mandevu alijaribu sana kuzuia ndoa ile lakini ilishindikana. Hamisa na Alitokea kumpenda sana Adrian Mbwana hivyo akajiomba radhi mwenyewe na akamwomba radhi mola wake kwa kuvunja taratibu za kidini.
"Kwa ninavyompenda Adrian. Sina jinsi kama ni kutengwa na familia basi sio shida ili mradi tu nafsi yangu iridhike.. Kwanza Adrian ni mzuri sana pili ana pesa nyingi sana zitakazotosha kubadilisha maisha yangu...!" Aliwaza Hamisa kisha akatabasamu.

Kwa kuwa Hamisa aliridhia kuwa Bwana Adrian hivyo akaolewa naye na akakubali kuifuata dini ya mumewe bila kinyongo kwani siku zote Mapenzi yakisema ndio hakuna anayeweza kupinga. Mapenzi yana nguvu kuliko sumu Kali inayoweza kuua, mapenzi yana nguvu kuliko kimbunga kinachoweza kuharibu makazi ya watu. Ni mapenzi hayohayo yaliyomfanya Hamisa kujitenga na ndugu zake na kuishi na Adrian.

Maisha ya ndoa kati ya Hamisa na Adrian yaliendelea kuwa ya amani na furaha. Na baada ta kuishi miezi mitatu Hamisa aliamua kurudi kwa wazazi wake ili kuwaomba msamaha kwani aligundua alikosea sana.
"Nikupe nini mke wangu mpenzi uende kwa wazazi?" Aliuliza Bwana Adrian.
"Nipe pesa ninunue zawadi ambazo zitawafaa..." Alisema Hamisa.
"Hakuna tatizo mke wangu.. Nakupenda sana" alisema Adrian na kumpa pesa kiasi mkewe ili afanye manunuzi ya zawadi na kuwaomba radhi wazazi wake.

Kesho yake Hamisa alivaa gauni refu pamoja na ushungi uliomsitiri vyema kisha akafunga safari kwenda nyumbani kwao. Aliongozana na dereva wake ambapo walifika mapema sana nyumbani kwao.
Hamisa alijawa na woga sana, alitembea taratibu sana mpaka alipochukua uamuzi wa kugonga mlango wa ndani. Hakuna aliyeitikia hodi yake ndipo Bwana Mandevu alipotokea nyuma akiwa ameshika mifuko michafu ya mkaa, Hamisa alitambua moja kwa moja kuwa baba yake alikuwa kwenye biashara zake za kuuza mkaa.
"Shkamoo baba" alisalimia Hamisa kwa woga kidogo. Bwana Mandevu alimtazama Hamisa bila kujibu salamu yake.
"Umefata nini hapa?" "Nimekuja kuomba radhi baba... Naomba tuingie ndani ili tuzungumze" alisema Hamisa.
"Wewe si una jeuri? Ondoka hapa kwangu... Sitaki uniabishe kama ulivyonitia aibu" alisema Mandevu kwa hasira. Hamisa aliamua kupiga magoti na kuzidi kumwomba radhi baba yake lakini Mzee Mandevu hakumwelewa kiurahisi.
"Baba unakumbuka kama ulinikubalia siku nilipokuambia nimepata mchumba?"
"Nilikubali kabla sijajua dini yake... Nilidhani ni mwenzetu katika imani kumbe sivyo... "
"Naomba basi nikuambie kitu"
"Kitu gani?"
"Mume wangu amebadili dini na amekuwa kwenye dini yetu... " alidanganya Hamisa ili kumshusha hasira baba yake.
"Unachosema ni kweli?" Aliuliza Mandevu akiwa amepunguza jazba kidogo.
"Ndio baba... Na tumefunga ndoa upya kabisa!" 
"Hayo ndio maneno... Haya karibu ndani..." Alisema Bwana Mandevu baada ya kumuamini haraka binti yake. Waliingia ndani na kuketi vitini.

"Mama yupo wapi?" 
"Alienda sokoni atarudi sasa hivi.." Alisema Bwana Mandevu kisha wakaendelea na mazungumzo mengine. Punde Mama Hamisa aliwasili nyumbani pale. Kwanza alishtuka kukuta gari imepaki nje ya nyumba yake akajiuliza sana.
"Gari hii imetoka wapi?" Kwani kwa kipindi kile magari yalimilikiwa na watu wachache sana wenye pesa nyingi. 
Mama Hamisa akaishia kuguna tu Kisha akaingia ndani kwake na kustaajabu alichokikuta kwani hakutaraji kama Hamisa angekuwa ndani ya nyumba ile.
"Hamisa!" Aliita kwa mshangao mama Hamisa.
"Abee mama... Asalam aleykum!" Aliitika Hamisa huku akitabasamu.
"Walleykum Salam! Umefika muda gani mwanangu mie!" Alisema Mama Hamisa huku akienda mbio kumkumbatia mwanae.
"Nilikukumbuka mno... Kila siku nilimwomba baba yako akusamehe tu" alisema mama Hamisa huku akiwa amemkumbatia mwanaye kwa furaha sana. Walikumbatiana kwa dakika kadhaa kisha 
Wakaachiana na wote wakaketi.
"Ile pale ni gari yako?"
"Ndio mama alinipa mume wangu.."
"Kuna MTU nimemwona kwa mbali kwenye ile gari ni nani"
"Ni dereva wangu nilimwacha ili asijue naongea nini na wazee wangu.." Alisema Hamisa huku tabasamu mwanana likiupamba uso wake.
"Mh mume wako ni tajiri sana eeh?"
"Kidogo tu.."
"Si kidogo... Mpaka amekupa gari?"
"Mke wangu... Mwanetu ameleta taarifa nzuri" alisema Mandevu huku akitabasamu.
"Zipi hizo?"
"Mumewe amekubali kubadili dini na wamefunga ndoa ya kidini" 
"Ya kweli hayo?"
"Ndio mama" alijibu Hamisa.
Kiukweli jambo lile liliwafurahisha sana na kuwafanya wawe na matumaini mapya ya kukomboa familia yao. Licha ya kwamba jambo lile halikuwa na ukweli wowote lakini lilibaki kuwa siri ya Hamisa pekee. 
Mama Hamisa aliandaa chakula wote wakala wakafurahi. Na kwa muda huo dereva aliitwa ndani na wakashiriki chakula kwa pamoja.
Hamisa aliwakabidhi wazazi wake zawadi alizowaletea na wakafurahi sana.

Baada ya chakula Mama Hamisa alimwita binti yake kwenye chumba kimojawapo ndani ya nyumba yao ile iliyochoka sana na kuonekana duni mno.

Baada ya Hamisa kuingia kwenye chumba kile chenye Giza kiasi, mama Hamisa akafunga mlango na kabla ya kuufunga alitazama huku na kule akahakikisha hakuna mtu aliye jirani.
"Hamisa mwanangu nilikasirika sana ulivokuwa mbali na Mimi... Nilitumia kila mbinu ili baba yako akusamehe ili wewe usiwe na kikwazo cha kuja hapa!" Alisema Mama Hamisa kwa sauti ya chini sana.
"Leo nimefurahi sana umekuja na sitokubali uondoke kabla hujakubali kufanikisha suala langu." Alisema Mama Hamisa kwa sauti ndogo.
"Kufanikisha suala lipi?" Aliongea Hamisa kwa sauti kidogo kuzidi ile aliyotumia mama yake.
"Ssh! Ongea taratibu kwani hii ni siri yangu Mimi na wewe! Baba yako hajui lolote"
"Sikuelewi..."
"Huelewi nini malaika wangu? Mbona tulishawahi zungumza kwani umesahau..?"
"Sikumbuki..."
"Usijali nitakukumbusha tu...." Alisema Mama Hamisa na kuinuka pale alipokuwa amekaa. Hamisa alikuwa na maswali mengi mno juu ya maneno ya mama yake ila hakuwa na haraka akasubiri kukumbushwa.

Mama Hamisa alisogea karibu na kona moja kisha akachimbua chini kwani nyumba ile ilikuwa haijasakafiwa hivyo kulikuwa na vumbi tu. Alipomaliza kuchimba pale chini akatoa kitu Fulani na kumsogelea Hamisa.
"Hamisa!"
"Nini hicho mama?" Hamisa alishtuka sana.

..................................
Itaendelea

No comments:

Post a Comment