Friday 9 September 2016

MSIMU WA PILI WA RIWAYA YA MWANAFUNZI MCHAWI SEHEMU YA 2

Riwaya:MWANAFUNZI MCHAWI (-2) MTUNZI:ENEA FAIDY SEHEMU YA 2 ....Hamisa alimshangaa mama yake huku akimtazama kwa woga. Mama Hamisa aliachia
tabasamu mwanana na kumtazama binti yake kisha kwa sauti ya upole sana akamnong'oneza. "Chukua ule mwanangu..ni zawadi yako." "Mmh! Mama!" Alisema Hamisa huku akisitasita kupokea zawadi ile anayopewa na mama yake. Kila alipojaribu kuinua mkono wake ukawa mzito kupokea akabaki ameduwaa tu huku akimtazama mama yake aliyejawa na tabasamu. Kutokana na giza lililokuwamo ndani mle Hamisa alishindwa kuona vizuri kitu alichopewa. "Hamisa! Kwasababu umeolewa na mume tajiri ndio chanzo cha kunidharau Mimi? Kumbuka Mimi ni mama yako... " alisema kwa sauti iliyoonesha kutopendezwa na tabia ya Hamisa. Na kutokana na upendo pamoja na adabu aliyokuwa nayo Hamisa katu hakutamani kumkwaza mama yake wala kumfanya ajisikie vibaya kwaajili yake. Ili kumridhisha mama yake Hamisa aliamua kupokea zawadi kutoka kwa mama yake kipenzi. "Aah kumbe ni apple!" Alisema Hamisa kwa mshangao huku akitabasamu na kupokea tufaha lile kubwa lililokomaa vizuri na kufanya rangi nyekundu ionekane vizuri kuliko kijani. "Sasa ulifikiri ni nini? Ni apple kwaajili yako mwanangu kipenzi" alisema mama Hamisa kwa furaha huku akihakikisha sauti yake haivuki nje ya chumba kile walichokuamo. "Sasa mbona ulilihifadhi chini ? Kwanini usiweke kwenye chombo kisafi?" Aliuliza Hamisa. "Utanikera na maswali yako.. Hebu kula haraka tutoke huku!" Alisema mama Hamisa kwa sauti ya ukali kidogo kwani aliufahamu vizuri utii wa binti yake hivyo akajua hatoendelea kudadisi zaidi. "Halijaoshwa mama.. Nitakula vipi?" Aliuliza Hamisa huku akikunja USO kwa kinyaa cha kula tunda chafu. "Kula hivyo hivyo binti yangu...jitahidi wala hakuna madhara yoyote!" Alisema mama Hamisa. Hamisa aliamua kumsikiliza mama yake na kula tufaha lile bila kuoshwa. Cha ajabu na cha kushangaza tunda lile lilikuwa tamu kupita kawaida hivyo likamhamasisha binti yule mrembo kula haraka haraka mpaka alipomaliza. Mara tu alipomaliza alihisi uchungu sana mdomoni mwake, uchungu ule ulikuwa zaidi ya Pilipili kichaa. Hamisa akabadilika uso akatamani kulia kwani alishindwa kuvumilia uchungu ule akataka kutema mate chini. Ghafla mama yake akamshika kinywa chake. "Usiteme mate hayo! Meza!" Alisema mama Hamisa. Ghafla sauti ya Mr Mandevu ikasikika ikiita kwa nguvu. "Mama Hamisa!" Lakini mama Hamisa hakutaka kuitikia akabaki kimya tu. "Mbona huitiki?" "Sitaki baba yako ajue nipo huku... Na usithubutu kumwambia chochote kuhusu tulichofanya sawa?" "Kwanini?" "Ni siri yetu.. Mimi na wewe na ukimwambia mtu mwingine yeyote utakuwa umeharibu kila kitu.." "Mbona sikuelewi mama... Apple lina tatizo gani" "Hahaha.. Ipo siku utafahamu. .. Vipi uchungu umeisha?" "Ndio ila kuna ukakasi kidogo.." "Usijali utaisha tu.. Ila nashukuru sana mwanangu umenitoa aibu..." Alisema mama Hamisa na kumfanya Mwanae abaki njia panda kwani kauli zile zilikuwa na utata sana kwake. Akajiuliza sana iweje tufaha lile Liwe na masharti mengi kiasi kile? Pia kwanini mama yake aseme limemtoa aibu wakati ni tunda la kawaida tu? Hamisa hakuwa jibu wala hakutaka kuuliza zaidi kwani mama yake alimwambia watoke chumbani mle haraka sana. Baada ya kutoka kwenye chumba kile walifika sebuleni na kuketi kama kawaida. Mandevu akamtazama binti yake ns kutaka kumuuliza jambo lakini ghafla akasita na kumuuliza jambo lingine mbali na alilokusudiwa. "We Hamisa kulikoni? Mbona upo hivyo?" Aliuliza. Hamisa akashtuka kidogo. "Nipo vipi?" "Mbona macho mekundu.. Halafu mdomoni kwako kuna damu?" Aliuliza Mandevu kwa mshangao. Hamisa alishtuka sana, lakini ghafla mama yake akamjibia maswali Yale. "Alijigongesha hapo nje... Kama umjuavyo mwanao kwa woga .. Si akaanza kulia" alisema Mama Hamisa kisha akamsogelea na kumfutafuta binti yake. "Mh! Inaonekana umeumia sana..!" Alisema Mandevu. "Ndio... Ila sasa hivi sina maumivu sana" "Oh! Pole..nataka mumeo aje huku ili tufahamiane zaidi maana ilikuwa kama ugomvi wala hatujawahi kukaa naye karibu hatujaongea chochote..!" "Sawa baba atakuja" alisema Hamisa. *** Hamisa alirudi kwa mumewe akiwa na furaha tele moyoni mwake kwani kupokelewa na wazazi lilikuwa Jambo jema sana kwake. Alimsimulia kila kitu mumewe na jinsi alivyowadanganya wazazi wake kuhusu dini ya mumewe. Lakini kwa suala hill Adrian alionekana kutokubaliana kabisa na mkewe. "Siwezi kukataa dini yangu.." Alisema Adrian. "Tafadhali mume wangu... Nakupenda sana, sitaki ndoa yetu iharibike kwaajili ya jambo hilo... Simaanishi kuwa utabadili dini ila cha msingi tu tuwaridhishe wazazi wangu... Nakuomba sana!" Alisisitiza kwa sauti ya kubembembeleza sana. Na kutokana ufundi wa kubembeleza aliojaaliwa Hamisa aliweza kumshawishi mumewe mpaka akakubali na wakapanga siku ya kwenda kuwatembelea wazazi wa Hamisa. Hamisa alizidi kuwa na furaha ingawa kuna jambo moja tu lilizidi kumtatiza na mara zote akifikiria basi amani yake ilipotea ghafla. Siku moja akiwa amekaa sebuleni akiwa peke yake ghafla akasikia kelele nyingi za vyombo jikoni kwake. Hamisa akainuka haraka na kwenda jikoni kutazams kilichokuwa kinaendelea. Na kadri alivyokuwa akisogelea ndivyo kadri alivyosikia vyombo vikianguka sakafuni na kuvunjika. Hamisa aliogopa sana. Akaingia jikoni na kutazama kabati la vyombo lakini cha kushangaza hakukuwa na chombo chochote kilichoanguka wala kuvunjika. Hamisa alipigwa na butwaa akaishia kushangaa tu kisha akarudi tena sebuleni. Aliporudi sebuleni Hamisa alishtuka tena baada ya kukuta vitambaa vyote alivyotandika kwenye sofa vipo chini, akakumbuka pindi anatoka aliacha vitambaa vyote vikiwa sehemu yake. Hamisa akapigwa bumbuwazi, akashangaa kwa muda kisha akajipa moyo kuwa labda upepo ulipiga kwa nguvu na kuangusha vitambaa. Hamisa akainama chini na kuokota vitambaa vyote na kuvirudisha sehemu yake. Hamisa akakaa tena kwenye kochi huku akiwa na mawazo tele kichwani mwake juu ya kile kilichotokea ndani ya nyumba yake. Akiwa katika mawazo hayo mazito ghafla usingizi ukamvamia na kumteka kwa mbwembwe nyingi. Hamisa hakuwa na ujanja ilibidi atii amri na kukubali usingizi umwendeshe kadri awezavyo. Mumewe akiwa ameambatana na mwanamke mmoja aliyevalia nguo nyeusi waliingia ndani na kufika sebuleni pale wakiwa wameshika visu huku wakimnyooshea Hamisa kifuani kwake. "Kumbe hunijui ee! Mimi ndo Adrian Mbwana... Naitaka roho yako haraka sana!" Ilisikika sauti ya Adrian akiongea kwa ukali sana. Hakuwa Adrian yule mpole, mnyenyekevu na mwenye mapenzi mazito ila alikuwa kama mnyama wa pori asiyejali uhai wa mtu. "Kaka usichelewe bwana.. Mchome kisu namimi namalizia" ilikuwa sauti Kali ya Dada yake Adrian akiwa hana hata chembe ya huruma. Adrian akakitazama kisu kile kirefu, chenye mng'ao wa shaba na kilichongoka vyema kwenye ncha ya mwisho ambayo ilimwelekea Hamisa. Adrian alikunja sura kikatili kisha akakibusu kisu kile na kukiinua kwa ghadhabu ili atue kifuani kwa Hamisa huku akiachia sonyo Kali ya dharau. Kabla kisu kile hakijamfikia Hamisa, Hamisa alishtuka sana usingizini huku akihema kwa nguvu sana. "Adriiiiiaaaaan!" Aliita kwa nguvu bila kutarajia lakini hakukuwa na mtu yeyote ndani ya nyumba ile zaidi yake yeye mwenyewe. Hamisa aliona kitini ni parefu sana akaamua kushuka na kukaa sakafuni huku akihema kwa nguvu. Woga ulimshika sana, akaangaza macho huku na kule Ili kutazama kama ndoto ile ina ukweli lakini bado hakuona chochote ndani ya nyumba ile wala hakukuwa na mtu mwingine yeyote. "Hii ndoto ina maana gani?" Alijiuliza Hamisa kisha akaanza kuunganisha matukio yote ya siku ile. Akakumbuka tukio la vyombo na vitambaa kisha akaunganisha na ndoto ile. "Niliambiwa Adrian ni mchawi... Anatumia uchawi katika biashara zake ili ziende vizuri..... Yawezekana kuna ukweli... Isije ikawa anapanga kuniua!" Aliwaza Hamisa huku kijasho chembamba kikimtoka kwa kasi sana usoni kwake. Aliwaza sana bila kupata majibu akiwa bado amekaa pale chini. Zilipita takribani dakika arobaini na Tano Hamisa akiwa katika dimbwi zito la mawazo. Ghafla akazinduliwa mawazoni na sauti ya mlango ukiwa unagongwa. Hamisa alishtuka, bado akasikia mlango ukigongwa. Taratibu alinyanyuka pale chini na kwenda kutazama nani alikuwa mgeni wake kwani hakuwa na wazo kama mumewe angerudi wakati ule kwani kikawaida mumewe alitoka kazini SAA moja jioni na akichelewa basi saa mbili. Na kwa muda ule ilikuwa ni saa Tisa alasiri. Hamisa alifungua mlango, alishtuka sana kuona mumewe akiwa ameambatana na mwanamke yuleyule aliyemuota. Tena wakiwa na mavazi yale Yale ya ndotoni. Mumewe alivalia Suti nyeusi, shati jeupe na tai nyekundu, mwanamke yule alivalia gauni refu jeusi na viatu vyeusi na alikuwa amejitanda mtandio mweusi. Moyo wa Hamisa ukampasuka paah! Akashinda hata kumkubatia mumewe kama ilivyokuwa kawaida yake! Kwani Siku zote Hamisa alimpokea mumewe kwa kumbatio zito la mahaba huku mabusu kama mvua yakimpoza uchovu bwana Adrian bila kujali aliambatana na nani lakini Siku hiyo hali ilikuwa tofauti sana.................................... JE NINI KITAENDELEA? USIKOSE KUFUATILIA.

No comments:

Post a Comment